Uongozi madhubuti wa serikali kupitia Mpango wa Taifa wa kudhibiti Kifua Kikuu (TB) na Ukoma (NTLP) umechangia kuongezeka kwa shughuli za TB ngazi ya jamii nchini kati ya 2005 na 2015 ambapo vikundi vya watu waliougua TB na kupona viliundwa katika wilaya 169. Wafadhili wa kimataifa kama vile Mfuko wa Dunia wa Kupambana na UKIMWI, Kifua Kikuu, na Malaria (The Global Fund), USAID, Stop TB Partnership, Chama cha Wagonjwa wa Moyo na Mapafu cha Norway (LHL) pia walichukua jukumu muhimu katika kuwekeza katika shughuli za Kifua Kikuu na kusaidia mashirika ya kijamii, asasi za kiraia na mashirika yasiyo ya kiserikali kutimiza wajibu wao katika kupambana na Kifua Kikuu nchini. NTLP pia ilichukua jukumu muhimu katika kuanzisha na kutekeleza mfumo wa ufuatiliaji na tathmini katika jamii ambao umefanikisha kuonyesha mchango wa jamii katika kuwabaini watu wenye maambukizi ya Kifua Kikuu. Ni kwa sababu hii kuanzia mwaka 2012, mwitikio wa jamii katika kupambana na Kifua Kikuu ulikabaliwa si tu jamii kuwa wahusika muhimu katika mapambano ya kitaifa dhidi ya Kifua Kikuu bali pia ilisaidia kupima mchango wake katika kufikia malengo ya Mpango Mkakati wa Kitaifa wa kutokomeza TB.

 

Hata hivyo licha ya kuwepo na muktadha mzuri wa kisiasa unaowezesha ushiriki wa jamii, kuongezeka kwa kasi kwa vikundi vya TB kulimaanisha kuwa mwitikio wa jamii katika kupambana na Kifua Kikuu nchini Tanzania ulitawanyika kutoka na kuwepo kwa vikundi na AZAKi nyingi. Kukosekana kwa jukwaa la pamoja la vikundi vya kijamii, mashirika ya kijamii, na mashirika yasiyo ya kiserikali ili kuratibu, kushirikiana na kubadilishana uzoefu kulifanya kila mdau kufanya kazi peke yake. Hali hii ilisababisha wadau mbalimbali kufanya shughuli zinazofanana katika baadhi ya maeneo na maeneo mengine kukosa wadau na kusababisha kujirudiarudia kwa njia zilizoshindwa kuchangia maendeleo katika eneo moja au mazingira sawa ya kijiografia. Ilimaanisha pia si tu kwamba vikundi na mashirika ya kijamii hayakuweza kuratibu kazi ili kubainisha upangaji na utekelezaji wa sera za kitaifa bali pia hayakufahamiana au kushirikiana kwa kiasi kikubwa.

 

Licha ya kuwa na idadi ndogo ya wadau katika jamii wanaoshiriki katika kukabiliana na Kifua Kikuu, ukosefu wa uratibu kati yao ulidhoofisha uwezo wao wa kushirikiana kimkakati na serikali na / au katika maendeleo ya sera ya kitaifa. Hali hii ilikuwa mbaya sana katika kuhamasisha mwitikio wa jamii katika kupambana na Kifua Kikuu nchini, ambayo ilidhoofishwa zaidi na ukosefu wa mifumo ambao ungeweza kuishirikisha serikali, washirika wa maendeleo, asasi za kiraia na wadau wengine katika shughuli mapambano dhidi ya Kifua Kikuu.

 

Ili kutatua changamoto tajwa hapo juu, mwaka 2016, Stop TB Partnership walifadhili zoezi shirikishi la Kubainisha Rasilimali za Jamii zilizoathiriwa na Kifua Kikuu kupitia mradi wa Challenge Facility for Civil Society. EANNASO ilichaguliwa kutekeleza zoezi la uandaaji wa ramani ya upatikanaji wa huduma kati ya Mei na Agosti 2016, ikizingatia ufikiwaji wa kijiografia na aina za huduma zinazotolewa pamoja na kiwango ambacho mahitaji yanayohusiana na Kifua Kikuu kwa watu walio katika mazingira magumu yalikuwa yametimizwa. Mazungumzo yalifanyika na jamii ili kuhakikisha mitazamo yao inazingatiwa katika uandaaji wa ramani. Hii ilichangia uelewa mzuri na wenye nguvu katika mwitikio wa jamii katika mapambano ya Kifua Kikuu nchini Tanzania, usanifu wake, wadau muhimu, uhusiano wao baina yao na tabia ya kushirikiana. Pia ilitambua fursa na mapungufu yaliyopo.


Matokeo yalithibitisha kuwa kulikuwa na wadau wachache wanaopambana na Kifua Kikuu, ni mashirika 16 tu yanayoshughulika na Kifua Kikuu pekee kwa nchi nzima, 35 yalishughulika na Kifua Kikuu na VVU, na 21 yalishughulika na masuala mtambuka. Kati ya mashirika 72, 10 yalikuwa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ya Kimataifa na 62 yalikuwa mashirika ya kijamii. Pamoja na mashirika yaliyosajiliwa, zoezi hilo liligundua vikundi 367 vya watu waliowahi kuugua Kifua Kikuu vilivyokuwa chini ya Mapambano ya Kifua Kikuu na Ukimwi Tanzania (MKUTA). Hatimaye, waligundua idadi kubwa ya watoa huduma za jamii wanaofanya kazi kwa kujitegemea kama Watoaji wa Huduma za Afya ya Jamii wa kujitolea katika ngazi ya kijiji.


Matokeo pia yalibainisha kuwa, wakati jamii zilihusika katika muitikio wa mapambano dhidi ya Kifua Kikuu, hazikuzungumza kwa sauti moja. Jamii ya watu walioathiriwa na TB hawakushirikishwa kikamilifu katika uandaaji wa sera, hii ilitokana haswa na ukosefu wa utaratibu ambao ungewezesha ushirikishwaji rasmi wa wadau tofautitofauti wa mapambano ya Kifua Kikuu katika maeneo tofauti ya kijiografia. Zoezi la uandaaji wa ramani lilipendekeza kuingizwa kwa mifumo ya kuboresha mawasiliano, uratibu na kuunda mtandao wa kuwezesha ushiriki rasmi na ulio sawa kwa taasisi za kiraia katika michakato ya kitaifa ya kukabiliana na Kifua Kikuu. Hii itasaidia kuongeza utetezi na kuleta matokeo mazuri ya utoaji wa huduma. Uratibu mzuri wa wadau wa Kifua Kikuu katika jamii ungewezesha utekelezaji wa ajenda ya utetezi katika ngazi ya kitaifa na ingeweza kupunguza mapengo ya huduma katika jamii, na pia kusaidia katika utoaji wa taarifa kuhusu njia sahihi za kukabiliana na Kifua Kikuu.

 

Matokeo haya yalitoa msingi wa ushiriki thabiti wa jamii na wa kimuundo ili kuhakikisha mwitikio mpana, jumuishi na unaozingatia haki katika kukabiliana na TB nchini Tanzania. Pia ilitoa uwazi zaidi na wadau gani wa Kifua Kikuu wapo na kuongeza nguvu kubwa kutoka kwa wadau ili kuanzisha mifumo muhimu ambayo itaimarisha mapambano dhidi ya Kifua Kikuu. Mnamo Juni 2017, miezi michache baada ya kukamilika kwa ramani, EANNASO na NTLP walifanya mkutano jijini Dodoma, ambapo washiriki kutoka zaidi ya AZAKi 30 waliamua kuunda Jukwaa la Jumuiya ya Kifua Kikuu nchini Tanzania yaani Tanzania TB Community Network (TTCN).